Warsha Ya Cotul, Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA)
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango jana tarehe 07 Novemba 2022 amefungua Warsha ya kitaaluma iliyoandaliwa na Shirikisho la Maktaba za Vyuo vya Elimu ya juu na Taasisi zinazofanya Utafiti (COTUL), ambayo itafanyika kwa siku tano katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella, mhandisi Ruyango amesema wanasayansi wamekutana pamoja kuzungumza kuhusu maktaba na utunzwaji wake pamoja na uwekaji wa vitabu vilivyoandikwa na Watanzania wazawa katika mfumo wa kiditajili ili viweze kusomwa kote duniani.
“Tuna Maprofesa wetu wameandika vitabu lakini ukienda kwenye mtandao havimo hii ni kutokana na mfumo tulionao, kupitia ‘National Digital Library’, tunaamini vitabu hivyo vitaingizwa, Watanzania wengi na wanavyuo wataanza kusoma vitabu viliyoandikwa na wazawa ndani ya mifumo ya dunia na mwisho tutanufaika kama Taifa na wale walioandika vitabu hivyo,” alisema Mhandisi. Ruyango.
Mwenyekiti wa COTUL, Dkt. Sydney Msonde amesema, dunia imebadilika na kila kitu kinafanyika kwa teknolojia, hivyo ipo haja ya kutoka analogia kwenda dijitali, huku akibainisha kuwa tafiti nyingi kwa sasa zinalenga kupata machapisho ya kielekroniki.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Cairo Mwaitete ametoa wito kwa wizara ya elimu sayansi na teknolojia kuwezesha miundombinu ya machapisho ya ndani (Local content) kupitia COTUL, ili kuwawezesha wanasayansi wa ndani waweze kuchapisha machapisho yao kwa gharama nafuu.
Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, Dkt. Mboni Ruzegea ametoa wito kwa waandishi wa machapisho ya ndani kuwasilisha machapisho yao katika Maktaba ya Taifa ili yaweze kuhifadhiwa
Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa wako katika mchakato wa kuanzisha sera ya huduma za maktaba nchini na kufanya marekebisho sheria ya huduma za maktaba ya mwaka 1975, ili iweze kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia; ambapo ameahidi kushirikiana na COTUL katika matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo.