Mafunzo Ya Maadili Kwa Watumishi IAA

Maaafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Arusha leo 05 Septemba 2022 wametoa mafunzo kuhusu rushwa na maadili kwa watumishi wa Umma katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Akiwasilisha mada hiyo Bw. Salum Nyamwese, Afisa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Arusha, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuwakumbusha wajibu wao kama watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.

Naye Mwanasheria Mwanandamizi TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Bi. Violet Machary ametoa wito kwa watumishi wa IAA kuhakikisha kuwa wanaepuka matumizi mabaya ya madaraka ili nafasi walizonazo ziweze kuwa na manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Akihitimisha mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete amewataka watumishi kuyatumia vema mafunzo hayo ili wasijihusishe  na vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ili kulinda taswira ya chuo na heshima yao kama wazazi.

“Taifa litajengwa na watu waadilifu ninyi watumishi ni kama wazazi na walezi kwa wanafunzi, mkiwa waadilifu mtakuwa kielelezo kwa wanafunzi ambao sisi tunawaandaa kuwa taifa bora la kesho,” alisisitiza Dkt. Mwaitete.