Pongezi IAA Ujenzi Wa Miradi Kwa Uaminifu, Uzalendo: Dkt Hawassi

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mlezi wa Vyuo na Vyuo Vikuu, Dkt. Frank Hawassi ameupongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu IAA kwa namna ulivyotekeleza miradi ya ujenzi kwa kutumia mfumo wa Force account kwa uzalendo na uadilifu.

Dkt. Hawassi ametoa pongezi hizo leo tarehe 17 Septemba, 2022 mara baada ya kutembelea miradi ya ujenzi wa majengo mbalimbali yaliyokamilika na yanayoendelea chuoni hapa.

"Kitendo cha kujenga majengo haya kwa gharama nafuu, ubora unatakiwa, mkitumia  mapato yenu ya ndani ni kazi nzuri tena ya mfano wa kuigwa na vyuo vingine; katika taasisi hii nimeona ubunifu, uaminifu, maona na uzalendo, endeleeni na moyo huu" alisema Dkt. Hawassi.

Aidha, Dkt. Hawassi amesema anatambua kazi zinazofanywa na Taasisi za elimu ya juu huku akiwaasa kutumia maarifa na weledi wao katika kuchochea maendeleo ya Watanzania bila kujali tofauti zao za  dini, kabila na kisiasa.

Awali akitoa taarifa kwa Kiongozi huyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete amesema ujenzi wa majengo hayo umekuwa na manufaa makubwa kwa chuo na jamii kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa vijana, kuongeza idadi ya wanafunzi ambapo kwa mwaka wa masomo 2021/2022 chuo kimekuwa na wanafunzi wapatao 10,350.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Epaphra Manamba amesema katika mwaka wa masomo 2022/2023 chuo kinatarajia kuwa na jumla wanafunzi 15,000