Maadhimisho Siku Ya Kimataifa Ya Uhasibu IAA

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeadhimisha rasmi siku ya kimataifa ya uhasibu leo tarehe 11 Novemba 2022. Maadhimisho haya yamefanyika Chuoni hapa yakijumuisha wakufunzi , wanafunzi na wadau wengine wa uhasibu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo kamishna msaidizi idara ya uendelezaji sekta ya fedha kutoka wizara ya fedha na mipango Bi Janeth Hiza amesema katika kuienzi siku ya kimatifa ya uhasibu ni muhimu wahasibu wazingatie maadili ya taaluma hiyo ili kuweza kujenga uchumi na kuleta maendeleo hapa nchini.

Bi. Hiza amesema kuwa Wizara ya fedha imeandaa programu ya elimu ya fedha kwa umma ili  kufikia mwaka 2025 asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa wa masuala ya fedha kwa lengo la  kusaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa masuala ya fedha, kutimiza malengo ya serikali na kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Wajumbe muhimu tunaowategemea kusaidia kufikisha ujumbe huu kwa umma ni walimu na wanafunzi kama ninyi, serikali imedhamiria watu waweze kuelewa masuala ya fedha, kuelewa ni maeneo gani wanaweza wakawekeza, nmna ya kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na maendeleo ya Taifa letu,” alisema Bi. Hiza.

Naibu Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Taaluma, Utafiti, na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Epaphra Manamba amesema lengo kuu la maadhimisho haya ni kutambua umuhimu wa taaluma ya uhasibu na kazi zinazofanywa na uhasibu katika taasisi mbalimbali.

Prof. Manamba ametoa wito kwa wahasibu wote kuzingatia uaminifu, taratibu, na miongozo ya uhasibu ili waweze kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya fedha na ukuaji wa uchumi nchini; huku akiahidi IAA kuendelea kutoa wataalam mahiri  watakaochangia maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Naye kaimu mkuu wa idara ya fedha na uhasibu-taaluma Dennis Hyera ameeleza kuwa siku ya uhasibu duniani imekuwa na manufaa katika kujenga mtandao na kufungua fursa mbalimbali kwa wahasibu nchini, huku akiwahimiza wahasibu kuendelea kudumisha kanuni na taratibu za kiuhasibu ili kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya fedha.

Makamu wa rais serikali ya wanafunzi IAA (IAASO) Shamza Edward ametoa rai kwa wanafunzi wenzake kuzingatia maadili ya taaluma zao wanayofundishwa wakiwa chuoni ili  watakapokwenda katika maeneo yao kazi wakafanye kazi zao kwa weledi.

Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhasibu hufinyika Novemba 10 kila mwaka na kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2022 inasema “Building Trust Enabling Sustainability’’.