Ziara Ya Waziri Wa Fedha Na Mipango Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA)

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba leo tarehe 25 Novemba, 2022 amefanya ziara katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na kutembelea miradi mbalimbali inayoendelea chuoni hapa.

Akizungumza na baadhi ya viongozi chuoni hapa Mhe. Waziri ameupongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kutokana na usimamizi bora wa fedha na ujenzi wa miundombinu ya majengo ya madarasa, ofisi na maabara za kisasa zinazojengwa kupitia mfumo wa ‘Force Account’.

’’Mradi huu hautabadilisha tu miundombinu ya Chuo bali unakwenda kubadilisha kabisa maisha ya watanzania, hivyo niwapongeze na ni vyema vyuo vingine viige mfano huu’’ alisema waziri.

Pia Mhe. Nchemba ameongeza kuwa maendeleo ya miundombinu yanayofanyika chuoni hapa yatasaidia ongezeko la wanafunzi wanaojisajili kujiunga na masomo ya elimu ya juu, hivyo yatachangia ukuaji wa sekta ya elimu kwa ujumla, na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

 Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mhe. Mrisho Gambo amemshukuru Mhe. Waziri kwa kufika Chuo cha Uhasibu Arusha na pia ameupongeza uongozi wa Chuo kwa usimamizi yakinifu wa miundombinu iliyojengwa na Serikali ikiwemo kisima cha maji kilichojengwa kwa ushirikiano wa Ufalme wa Nchi za Kiarabu (UAE).

 Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete ametoa shukrani kwa Waziri, Serikali, Wizara ya Fedha na wadau mbalimbali kwa ujumla kwa kuunga mkono ujenzi wa miundombinu iliyopo na inayoendelea kujengwa chuoni hapa.  Dkt Mwaitete ametaja miradi mikubwa inayoendelea kujengwa kwa sasa ikiwemo madarasa pamoja na ujenzi wa ‘Hostel’ 4 zenye uwezo wa kulaza wanafunzi 2000.

 Ziara hii imeambatana na uzinduzi wa kisima cha maji uliofanywa na Mhe. Waziri Nchemba kilichojengwa katika Chuo cha Uhasibu Arusha kwa juhudi za Serikali kupitia Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo kwa ushirikiano na Falme za Nchi za Kiarabu (UAE).