Mafunzo Ya Usalama Wa Mtandao

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),
Dkt. Cairo Mwaitete amefungua mafunzo ya siku tano ya usalama wa mtandao
yanayofanyika chuoni hapa, kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa
TEHAMA kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa mtandao.
Akifungua mafunzo hayo Dkt. Mwaitete amesema kutokana na uwepo wa mashambulizi ya kimtandao (cyber-attacks) ikiwemo udukuzi, uelewa wa masuala ya usalama wa mtandao ni muhimu kwa wataalam ili waweze kuyakabili na kuhakikisha usalama wa taasisi na Taifa kwa ujumla.
“Tunahitaji wataalam mahiri wenye weledi ambao watalinda taasisi zao na Taifa, usalama wa mtandao ni eneo nyeti kwa usalama wa taasisi na Taifa na ndiyo maana mko hapa kupata maarifa haya”, alisema Dkt. Mwaitete.
Aidha, amewataka kutumia vizuri muda wao wa mafunzo kubadilishana uzoefu katika utaalam wao, kuhakikisha wanakusanya taarifa zote muhimu kutoka kwa wawezeshaji ili wakaimarishe utendaji wao.
Mratibu wa mafunzo Bi. Josephine Shirima
kutoka Mtandao wa Elimu na Utafiti Tanzania (TERNET), amesema mafunzo hayo
yamewakutanisha wataalam wa TEHAMA kutoka
taasisi mbalimbali nchini; lengo likiwa kuwajengea uwezo katika usalama
wa mtandao kwenye utambuzi wa mashambulizi ya kimtandao na kukabiliana nayo
kabla hajaleta madhara.