Mdahalo wa Mmomonyoko wa Maadili

Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeandaa mdahalo uliojikita katika suala la mmomonyoko wa maadili kwa lengo la kutoa elimu kwa jumuiya ya chuo na jamii kwa ujumla, hili kusaidia kuzuia ukatili wa kijinsia na vitendo vingine viovu ambavyo kwa sehemu kubwa vinasababishwa na mmomonyoko wa maadili

Akifungua mdahalo huo Afisa Maendeleo ya Jamii jiji la Arusha Bi. Habiba Madebe akimuwakilisha mgeni rasmi Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Arusha, amesema sababu mojawapo ya ukatili wa kijinsia ni mmomonyoko wa maadili ambao unapelekea kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Vilevile Bi. Habiba ameupongeza uongozi wa Chuo Cha Uhasibu Arusha kwa kuanzisha dawati la jinsia, kwani wamekuwa sambamba na mikakati ya serikali kutokana na kuzinduliwa miongozo mbalimbali ya kupambana na ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto.

Naibu Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Epaphra Manamba ameeleza kuwa uongozi wa IAA umekuwa ukiendesha mijadala ya kutoa elimu kwa wanafunzi na wafanyakazi, hili kuhakikisha wanaiunga mkono serikali katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wao viongozi mbalimbali wa dini waliohudhuria katika mdahalo huo wamesema, familia ndio sehemu pekee inayoweza kujenga au kubomoa maadili hivyo amewahasa wazazi kuwafundisha, kuwaelekeza, kuwahudumia, na kuwapenda watoto wao, pia kumtanguliza mwenyenzi Mungu mbele ili kuandaa jamii bora itakayokemea ukatili wa kijinsia.

Nae wakili kutoka (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha Bi. Violet Machary ameeleza kuwa mmomonyoko wa maadili unapelekea athari mbalimbali ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, hivyo amewahasa washiriki wa mdahalo huo kuwa ni vyema kuuthamini utu wao na kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa faida ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Mdahalo huo umefanyika katika Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) ukujumuisha wanafunzi na wafanyakazi wa chuo, viongozi wa dini, pamoja na watoa mada kutoka taasisi mbalimbali za serikali ikiwa ni moja ya mijadala inayoendelea kuelekea kilele cha maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.