Career Day IAA 2023

Chuo cha Uhasibu Arusa (IAA) kila mwaka huandaa siku maalum kwa wanafunzi kuonesha ujuzi na vipaji vyao yaani (IAA Career Day) kwa wadau mbalimbali katika sekta wanazosomea, mwaka huu siku hii imeadhimishwa leo Chuoni hapa. ikiwa na kauli mbiu “Discover your strengths, Unlock your Career Opportunities”.

Akizungumza na wanafunzi katika Career day leo Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini Bi. Chiku Issa amesema IAA ina vijana wenye vipaji na ubunifu ambao wanahitaji kusaidiwa kifedha kwa kupewa mikopo ili kufikia ndoto zao.

“Naipongeza menejimenti ya Chuo kwa kuwapa fursa vijana kipitia ‘incubator’ yao, wanatekeleza kwa vitendo yale ambayo serikali imekuwa ikiyasemea, kwamba ajira zinaweza kutengenezwa na vijana wenyewe, kwa kuwa nafasi za ajira za kudumu ni chache; hivyo naahidi kuungana na chuo kuwasaidia vijana hawa kifedha,” alisema.

Akimwakilisha Mkuu wa Chuo IAA, Naibu mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala, Dkt. Cairo Mwaitete amesema wanafunzi walioonesha vipaji vyao katika teknolojia, ujasiriamali na Sanaa wamedhihirisha IAA inafundisha kwa kuzingatia umahiri, ili kuendana na soko la ajira; hivyo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaleta watoto wao IAA ili wapate elimu bora.

Mshindi wa kwanza kundi la ujasiriamali Bw. Mukhammad Costa amesema amepata mafanikio akiwa IAA na mpaka sasa amefungua kampuni na kumuwezesha kujiajiri na kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana wengine saba.

Career day mwaka 2023 imehusisha maonesho ya kazi mbalimbali za vipaji, ubunifu na uvumbuzi kwa wanafunzi kutoka katika fani mbalimbali, ambazo zilishindanishwa katika makundi matatu yaani teknolojia, ujasiriamali na Sanaa.

Akitangaza majina ya wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika makundi hayo Jaji Mkuu wa mashindano hayo Neema John amesema wamepatikana washindi watatu kwa kila kundi ambapo kundi la ujasiriamali limeongozwa na Mukhammad Costa, kundi la teknolojia ni Allen Kileo na kundi la Sanaa ni Kareen Kamene.