Maadhimisho ya Siku ya Bima IAA

Chuo Cha Uhasibu Arusha IAA leo tarehe 02 Juni 2023  kimeadhimisha siku ya Bima (Insurance Day) duniani iliyofanyika chuoni hapo, ikiwa na kaulimbiu inayosema “My life, My Wealth, If Insured it will be safe’’.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kanda ya kaskazini Bi Gladness Lema ameipongeza IAA kwa kuanzisha kozi za Bima na kuahidi kuwa  taasisi hiyo itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha wanapatikana wataalam mahiri na wenye weledi.

Bi Gladness ameongeza kuwa kwa sasa ni asilimia 18 ya Watanzania wanaotumia bima, hivyo soko la bima na taifa kwa ujumla linahitaji wataalam wengi zaidi wa bima waadilifu na wenye weledi ili waweze kuwafikia Watanzania wasio na elimu ya bima.

‘’Sitegemei mwanafunzi atakayehitimu katika sekta ya bima aanze kutembea na bahasha kutafuta ajira, kwa sababu anaweza kujiajiri hata bila mtaji, akishirikiana na makampuni yaliyosajiriwa na TIRA, pia ni sekta inayolipa zaidi na inaajiri vijana wengi,”

Naye Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Taaluma, Utafiti, na ushauri wa Kitaalamu Prof. Epaphra Manamba ameeleza kuwa wana programu za bima kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada, na mpaka sasa wana  wanafunzi wapatao 390 wanaotarijiwa kuhitimu kwa mara ya kwanza mwaka 2023.

Prof. Manamba ameongeza kuwa programu za bima IAA zinatolewa kwa mfumo wa uanagenzi (apprenticeship) ambapo mwanafunzi anasoma asilimia 50 darasani na asilimia 50 nyingine anasoma kwa vitendo katika maeneo ya kazi (field), hivyo huwawezesha kuwa na ujuzi pamoja na uzoefu wa kazi.

Mdau wa bima kutoka Arusha Bw. Peter Kilasara ameeleza kuwa bima ni muhimu katika kusaidia  watu kujilinda na athari za majanga mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na jamii kwa ujumla, hivyo elimu hii inawaandaa  wanafunzi kupata ujuzi kuhusu masuala ya bima ili wakatoe elimu kwa jamii.

Mwenyekiti wa IAA Insurance Club Martin Hoka ameushukuru uongozi wa IAA kwa elimu wanayowapatia iliyowafanya kuwa mfano bora katika taasisi walizoshirikiana nazo katika mafunzo kwa vitendo, hivyo kuwa wajuzi na wabobezi katika masuala ya bima

Maadhimisho haya yaliyofanyika kwa mara ya kwanza yamehudhuriwa na wanafunzi, wafanyakazi wa IAA, wadau mbalimbali wa bima zikiwemo taasisi za serikali na zisizo za kiserikali.