Maadhimisho Ya Siku Ya Wanawake Duniani Mwaka 2024

Wanawake wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kutoka katika Kampasi zake za Arusha, Babati, Dar es Salaam na Dodoma Leo tarehe 08 Machi, wameungana na Wanawake wenzao nchini kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika mikoa yao.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Mkoani Arusha, katika Viwanja vya Ngarenaro, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Emmanuela Kaganda ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela,  amesema lengo la maadhimisho haya ni kuwezesha utekelezaji wa kauli mbiu ya kuwekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Mhe. Kaganda amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuhakikisha kuwa Wanawake wanapewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali ikiwemo kumuinua mwanamke kiuchumi na kisiasa.

"Katika kuboresha sekta ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, serikali imehakikisha wanawake wanashiriki shughuli za kiuchumi na kunufaika na fursa zilizopo serikalini na kwa wadau mbalimbali, ikiwemo uundwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika ngazi zote za kiutendaji," amesema Kaganda.

Mhe. Kaganda amesema pamoja na kujiimarisha kiuchumi,wanawake wanapaswa kuzingatia jukumu la malezi ya watoto na familia ili kuwa na jamii yenye maadili mema na maendeleo jumuishi.

Aidha, Kaganda ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Naye Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake mkoa wa Arusha, Bi. Sifa Swai amewahimiza wanawake kutenga muda wa kuzungumza na watoto na kuwashirikisha wanaume katika malezi na makuzi ya watoto, ili kupunguza masuala ya ukatili kwa watoto yanayoendelea kwenye jamii.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2024 ni: "Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo na Ustawi wa Jamii."